Wednesday, November 3, 2010

Siku ya kuwaombea waamini marehemu wote: Kifo ni mwanzo wa maisha mapya katika Kristo!

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba, anawakumbuka waamini wake marehemu wote waliolala katika usingizi wa amani wakiwa na tumaini la uzima wa milele.

Akizungumza na waamini na mahujaji waliohudhuria kwenye Sala la Malaika wa Bwana, katika maadhimisho ya Siku kuu ya watakatifu wote, kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, kifo ni jambo linalosababisha majonzi na machungu, lakini kwa waamini wenye imani na matumaini hawana haja ya kuogopa fumbo la kifo katika maisha yao, kwani wanaunganishwa kwa namna ya pekee na Kristo aliyeshinda dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, jana majira ya jioni, alitarajiwa kwenda kusali chini ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Mababa watakatifu waliozikwa chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na kuwaombea marehemu wote.

Tarehe 4 Novemba, nyakati za asubuhi, ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea marehemu Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2009 - 2010.

Kifo ni mwanzo wa maisha mapya katika Kristo na kama kuna jambo ambalo mwanadamu ana uhakika nalo ni juu ya kifo. Ndiyo maana Mheshimiwa Padre Nicodemus Hindoy kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano, kilichoko mjini Roma hasiti kuwaita "marehemu watarajiwa", changamoto kwa kila mwamini kujitahidi kufa katika hali ya neema ili aweze kuurithi uzima wa milele.

Ninakualika sasa ujiunge naye Mama Kanisa anapotolea siku ya tarehe 2 Novemba na kwa namna ya pekee Mwezi Novemba kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watoto wake waliolala katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini la ufufuko katika wafu.

Ndugu zangu tunapowakumbuka marehemu wote, na kuwaombea kwa namna pekee, hasa wale ambao hawana waombezi, tunapata nafasi ya kutafakari jukumu la kila mmoja katika ushirika na kila mbatizwa, awe bado yuko hapa duniani, toharani, na hata wale ambao tayari wanashiriki utukufu wa milele yaani ambao hapo tarehe 1 Novemba, tumeadhimisha Siku kuu ya watakatifu wote.

Kanisa Katoliki linafundisha kwamba, kuna makundi matatu ndani ya kanisa la Mungu, kanisa linalosafiri, yaani sisi tuliopo duniani, kanisa linalotakaswa, yaani wale waliopo katika hali ya kutakaswa – waliopo toharini na Kanisa lililopo mbinguni yaani watakatifu.

Tarehe 2 Novemba, Kanisa la duniani kote linaungana kwa sala na kanisa la toharani, ili pamoja nao kwa njia ya sala zetu waweze kushirikishwa ule utukufu tunaoutamani kuurithi milele. Ni imani yetu kuwa mtu anapofariki katika hali ya neema lakini bado ana mapungufu madogo madogo, anashiriki hali ya kutakaswa, si sahihi kuwahukumu wenzetu waliotutangulia kwa mapungufu Fulani Fulani, kwani huruma ya Mungu na Utakatifu wake hauna mipaka, siku zote anakuwa sikivu kwa sala na maombi ya wana wake: hapo ndipo sala zetu na nia zetu njema zinapopata nafasi katika kutakaswa kwao, Mungu daima anakuwepo na anazikubali sala na nia njema ya watu wake.

Ndio maana mtakatifu Paulo katika barua yake kwa Wafilipi 1:21 anatushawishi kuwa tujirudi na kuikubali maana sahihi ya kifo, kwamba kifo hakitutenganishi na wenzetu katika Kristu, wala na Kristu mwenyewe, na kwamba sisi tukifa tunakufa katika Kristu na tutaishi naye, kumbe baada ya ubatizo wetu hakuna kinachoweza kututenganisha katika umoja aliotuombea Kristu kwamba tuwe na “umoja kama wao UTATU MTAKATIFU walivyo wamoja”.

Tunaalikwa kuona kuwa kifo si mwisho wa maisha bali ni mwanzo wa maisha mapya katika Kristu, maisha ambayo sina shaka kila mwanadamu mwenye akili timamu anayatamani kuyarithi. Sala zetu na sadaka zetu zina thamani ya pekee mbele za Mungu na kwa ajili ya ndugu zetu waliotoharani. Hatuzungumzii kuyabadili mawazo ya Mungu au kumhonga Mungu kwa sadaka na sala zetu kama wengine wanavyotufikiria katika siku hii tunapowaombea ndugu zetu marehemu, kitu cha msingi na cha uhakika ni nia yetu njema katika sala, sadaka na maombezi kwa ajili ya ndugu zetu.

Ni ukweli usiopingika kwamba katika umoja wetu na ndugu zetu marehemu na watakatifu Mungu anakuwepo kati yetu, anazibariki na kuzikubali nia zetu. Kumbe kuwaombea marehemu ni tendo la kiimani, na tunapaswa kufanya kwa imani na kwa hakika itazaa matunda mema katika imani, tusonge mbele na nia yetu njema katika hili, bila aibu na hofu yoyote, sisi tunaamini na tunajua kwa nini tunafanya hivyo.

Tunapowakumbuka ndugu zetu marehemu, tukumbuke kwamba na sisi ni marehemu watarajiwa ili tufe katika hali ya neema inayotakiwa katika kuurithi uzima wa milele. Kama kuna jambo tunalopaswa kuwa na uhakika nalo ni kufa, kumbe tunapaswa daima kuwa tayari, kwa sababu hatujui siku wala saa atakapotuita Mungu toka maisha haya.

Ni bahati mbaya hatupendi kusika neno kufa katika maisha yetu licha ya kulizungumzia, lakini cha kushangaza ukimwuliza mtu kama anapenda kwenda kwa Mungu kila mmoja anapenda awe ya imani gani, tunasahau kuwa hatuwezi kurudi kwa Mungu bila kufa, na kufa ni mabadiliko ya ghafla ya maisha ya sasa na kuingia katika maisha ya milele tukifa katika neema ya Mungu.

Tuyabadili maisha yetu yasiyompendeza Mungu, ili tuweze daima kutembea katika neema zake na tufe katika neema zake, tuwe na ushujaa kama wa mtakatifu Paulo kwamba kuishi kwake ni Kristu, na kufa ni faida, tukiwa na msimamo huo tutaelewa vizuri nini maana na sababu ya kuwa kwenye umoja na ndugu zetu marehemu. Tuendelee kuwakumbuka daima ndugu zetu marehemu ili Mungu awaonyesha uso wake wa huruma na hatimaye kurithi utukufu wa milele. Source: Radio Vatican

1 comment: