Wednesday, January 12, 2011

MKUTANO MKUU WA 3 WA WANA-SPS

TAARIFA YA GOMBERA KWA WANA SPS
 MSIMBAZI CENTRE, DAR ES SALAAM 
TAREHE 12/01/2011


1. UTANGULIZI:

Waheshimiwa wana SPS, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kutujalia kufika siku ya leo tunapokusanyika hapa kwa lengo la kupeana taarifa muhimu juu ya maendeleo ya mama yetu SPS.

Tunatambua majukumu mengi mliyonayo lakini kutokana na upendo wenu wa dhati kwa seminari yetu, mkitambua mchango mkubwa wa shule hii kwenu mkawa tayari kutenga muda kwaajili ya mama SPS.  Tunasema asanteni sana na Mungu awabariki kwa utayari na upendo wenu kwa mama yetu.

2. TAARIFA YA SEMINARI:

Waheshimiwa wana SPS, Seminari Ndogo ya Mt. Petro, Morogoro ni    shule ya kikatoliki inayotoa elimu ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha    sita na malezi maalumu ya kidini na kimaadili kwa vijana wanaoandaliwa    kuwa Mapadre wa Kanisa Katoliki.

Shule hii inamilikiwa kwa pamoja na Majimbo Saba ya Kanisa Katoliki    ambayo ni Dar Es Salaam, Zanzibar, Morogoro, Tanga, Same, Mahenge na    Dodoma.  Kwa ruhusa maalum ya Mwenyekiti Bodi ya Maaskofu tunaopia     waseminaristi kutoka Jimbo Kuu la Songea, Mashirika ya Wasalvatori,    Wabenedictine na Wakarmaleti.

Kwa sasa seminari ina idadi ya wanafunzi 355.


2.1. MAENDELEO YA TAALUMA:

Waheshimiwa wana SPS, Seminari yetu bado ni moja kati ya shule bora Tanzania kwa wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao ya Taifa.  Pamoja na ukweli kuwa kwa muda mrefu hatujaingia katika kumi bora.

Hata hivyo jitahada zinafanyika kwa kiwango kikubwa kwa ushirikiano wenu ili tuirudishe seminari yetu katika kumi bora kitaifa.

Hadi sasa tunapoanza mwaka huu 2011 shule imekamilisha kuwa na idadi sahihi ya walimu wanaohitajika, tena ni walimu wanosifika kwa ubora.

Bado zoezi la kuboresha maktaba yetu na mahabara linaendelea. Tunaamini baada ya muda mfupi tutaweza kurudi kileleni tulipokuwa miaka ya nyuma.

2.2. CHANGAMOTO:

Waheshimiwa wana SPS, Utume wa Seminari Ndogo ya Mt. Petro, Morogoro  tangu iasisiwe ni kutoa elimu bora ya sekondari na malezi bora kwa vijana wenye mwelekeo wa kuwa mapadri kwa gharama nafuu inayoweza  kulipwa na hata familia zenye kipato kidogo sana.  Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, Morogoro ni moja ya shule zenye kiwango kidogo sana cha ada miongoni mwa shule binafsi za bweni.

Kwa sasa kiwango cha ada kinachotolewa kinakidhi 70% ya gharama za kawaida za kuendeshea shule bila kuingiza mipango ya maendeleo na ukarabati mkubwa.  Hii  inamaana kwamba 30% ya gharama za kuendesha shule lazima zipatikane  kutoka vyanzo vingine kama miradi ya shule na misaada ya wahisani.

Mara nyingi shule imeshindwa  kupata hiyo 30% ya bajeti toka vyanzo hivyo.  Misaada ya wahisani haizidi 15% ya bajeti ya shule; na miradi ya shule  inachangia 2% tu ya bajeti hiyo.  Mbaya zaidi, karibu kila mwaka karibu wanafunzi 20 hushindwa kabisa kulipa ada, hii ni sawa na 4% ya bajeti ya shule.  Hii inamaana kuwa kila mwaka, shule inakuwa na upungufu wa 17% katika bajeti yake na hii ni kwa ajili ya gharama za kawaida tu za kuendeshea  shule, bila kuingiza mipango ya maendeleo na ukarabati mkubwa.


Hivyo pamoja na nia nzuri ya seminari kutoa elimu na malezi bora kwa gharama nafuu, seminari imejikuta katika wakati mgumu kiuchumi .  Bajeti ya shule inakuwa ndogo na hivyo kuathiri mambo mengi, kama vile:

·        Kukosa uwezo wa kuboresha chakula cha wanafunzi;
·        Kukosa uwezo wa kutoa mishahara mizuri kwa walimu na wafanyakazi wasio walimu;
·        Kukosa uwezo wa kukarabati mejengo ya shule na kuyaweka katika hali bora;
·        Kukosa uwezo wa kununua vitabu vya  kiada na rejea vya kutosha kwa matumizi ya wanafunzi na walimu; na
·        Kukosa uwezo wa kuboresha darasa la kompyuta.

2.3. MATAZAMIO YETU:

Tukiwa na  uchumi imara seminari itakuwa katika nafasi ya kuendelea na utume wake wa kutoa elimu bora ya sekondari na malezi bora kwa vijana wenye muelekeo wa kuwa mapadre kwa gharama nafuu inayoweza kulipwa hata na familia zenye kipato cha chini sana.

Hivyo, wakati seminari inaendelea  kusisitiza na kukusanya ada kutoka kwa wanafunzi, wakati seminari inabuni na kutekeleza miradi ya kiuchumi, ni muhimu kwetu kuomba wahisani ndani na nje, mashirika, vikundi na mtu mmojammoja  ambao wnaamini katika utume wa seminari hii ili waungane nasi katika utume huu.

Tunawashukuru sana wana SPS (St. Peter’s Seminary Alumni) ambao  kwa namna  ya pekee tumeamua  kusaidia  maendeleo ya seminari yetu. Kwa muda mfupi wa mwaka mmoja tangu tulipoanza rasmi kutekeleza azma hiyo hapo January 12, 2010 tumeisaidia seminari kwa mambo mengi kama vile:-

·        Kununua meza mbili za mpira wa meza (table tennis) na seti zake (rackets) vyenye kiwango cha Olympics vyote vikiwa na thamani ya Tshs 1,431,000.-
·        Kugharimia magoli ya uwanja wa mpira wa miguu (Tshs 613,750.-)
·        Kuchangia uanzishwaji upya wa shamba la  matunda,  tayari miche elfu moja (1000) ya michungwa na miembe imeshapandwa. Alumni tumechangia Tshs 250,000.- sawa na miche 100.
·        Vitabu vya kiada na rejea vyenye thamani ya Tshs. 6,376,000.- vimenunuliwa na kutolewa zawadi kwa seminari.
·        Meza 13 za mninga na viti vya kisasa vya ofisini 23  vyenye thamani ya Tshs 1,875,000.- vimetolewa zawadi kwa seminari.
·        Mradi wa Biogas wenye thamani ya Tshs 13,973,300.-           umeshaanza kutengenezwa kwa matumizi ya jiko la wanafunzi.

Jumla ya mchango wote wa wana SPS ni Tshs 24,519,050.-  sawa na 7.8% ya bajeti ya shule kwa mwaka 2010. Ni msaada mkubwa sana kwa seminari yetu, tunawashukuru sana.

2.4. MKAKATI  WA KIUCHUMI:

Waheshimiwa wana SPS, ili kukabiliana na  changamoto za kiuchumi zilizopo mbele yetu, pamoja na jitihada nyingine seminari imeanzimia kwa mwaka huu 2011 kuboresha mradi wa nguruwe kama mpango wa kujinasua kiuchumi.
Lengo letu ni kuwa na nguruwe 228. Kwa sasa mabanda yetu yana uwezo wa kuchukua nguruwe 128; kufikia lengo la kuwa na nguruwe 228 tumeazimia kuongeza banda la kuchukua nguruwe 100 zaidi.

Kwa zoezi hili tunatazamia kuboresha chakula cha wanafunzi na kupata pato ambalo kwa pamoja kwa gharama za mwaka wa kwanza wa mradi ni sawa na faida ya Tshs 14,153,053.- kwa mwaka, sawa na 4.5% ya bajeti ya shule.

Ujenzi wa banda jipya la nguruwe utagharimu    Tshs   9,403,425.-
Huduma (chakula na madawa, n.k.)                     Tshs 17,651,760.-
                   Gharama ya mradi                          Tshs 27,055,187.-

Wakati tukiendelea kutafuta wahisani wa kutusaidia ujenzi huo, tayari tumeshaanza kuboresha mifugo iliyopo na kuongeza idadi ya nguruwe ili kujaza mabanda yaliyopo. Hadi sasa shule ina nguruwe 100 wa umri tofauti.


2. 5. MWISHO:

Safari ni ndefu na magumu ni mengi, lakini tutafanikiwa kama  tukizingatia     msemo wa kiswahili “umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”

Kwa moyo wa dhati tunawomba wote wenye kuamini na kuthamini pamoja     nasi utume wa seminari hii tuendelee kuwa kitu kimoja tuiendeleze     seminari yetu.  “Penye  nia pana njia”.  Tukifanya  kazi bega kwa bega kwa     ushirikiano wa dhati tutaifanya seminari hii kuwa bora katika kila nyanja na     hivyo kutoa wahitimu bora watakaolitegemeza  kanisa na jamii kwa ujumla.

3. HITIMISHO:

Napenda kuhitimisha taarifa hii kwa kuwashukuru tena Waheshimiwa wana SPS kwa kuuenzi umoja huu na kuithamini shule yetu,  Mungu awabariki     sana. Salamu nyingi toka seminarini.


No comments:

Post a Comment