1. UTANGULIZI:
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kutujalia kufika siku ya leo tunapokusanyika hapa kwa lengo la kuwaaga vijana wetu wa kidato cha nne.
Pia kwa niaba ya Jumuiya ya Seminari Ndogo ya Mt. Petro, Morogoro napenda kukukaribisha wewe Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Padri Romanus Dimoso, Daktari wa uchumi na Mkufunzi Chuo Kikuu Mzumbe na pia kukushukuru kwa utayari wako wa kuitikia mwito wetu wa kuja kuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali haya ya 41 ya kidato cha nne. Ukiwa Tunda la Seminari hii, uwepo wako hapa hakika unaleta changamoto na faraja ya pekee kwetu na tunaona kuwa kazi inayofanywa na Seminari hii haipotei bure.
Tunatambua unayo majukumu mengi pale chuoni lakini kutokana na upendo wako wa dhati kwa Seminari hii, ukitambua mchango mkubwa wa shule hii kwako ukawa tayari kutenga muda kwa ajili yetu. Tunasema asante sana na Mungu akubariki kwa utayari na upendo wako kwetu.
Aidha tunawashukuru wageni wote mliofika siku hii ya leo, waheshimiwa Mapadri na Watawa, marafiki wa Seminari, Kamati Tendaji ya St. Peter’s Seminary Alumni, wazazi na walezi. Ujio wenu unaleta furaha na tumaini jipya kwetu kwani ni ishara ya mshikamano katika suala zima la malezi ya wito wa upadre, kuijenga na kuendeleza Seminari yetu.
2. TAARIFA YA SEMINARI:
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Seminari Ndogo ya Mt. Petro, Morogoro ni shule ya Kikatoliki inayotoa elimu ya sekondari Kidato cha Kwanza hadi cha Sita na malezi maalumu ya kidini na kimaadili kwa vijana wanaoandaliwa kuwa Mapadre wa Kanisa Katoliki.
Shule hii inamilikiwa kwa pamoja na Majimbo saba ya Kanisa Katoliki ambayo ni Dar Es Salaam , Zanzibar , Morogoro, Tanga, Same, Mahenge na Dodoma . Kwa ruhusa maalum ya Mwenyekiti wa Bodi ya Maaskofu tunao pia Waseminaristi kutoka Jimbo Kuu la Songea, Mashirika ya Wasalvatori, Wabenedictine na Wakarmeli.
Kwa sasa Seminari ina idadi ya wanafunzi 324, wakiwemo vijana 14 wa kidato cha nne tunaowaaga leo.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tunapofanya mahafali haya ya 41 ya Kidato cha Nne, Seminari hii inatimiza miaka 41 tangu iwepo hapa Morogoro. Kihistoria Seminari hii ilianza huko Ilonga, Wilayani Kilosa mwaka 1936, ikahamia Bagamoyo na mwaka 1969 ikahamishiwa hapa ilipo sasa.
2.1. MAFANIKIO:
Kwa kipindi cha miaka 41 tangu Seminari ihamie hapa Morogoro, Seminari imekuwa na mafanikio makubwa katika nyanja mbali mbali hasa katika kutoa wahitimu kwani hadi kufikia leo tarehe 16.10.2010 Seminari imeweza kutoa wahitimu 2104 na kati yao 215 ni mapadri na kati yao watatu ni Maaskofu.
Ni habari njema pia kuona kuwa wale ambao hawakufikia lengo la kuwa Mapadre wamekuwa hazina njema kwa jamii ndani na nje ya Tanzania .
Seminari imetoa watu katika medani mbalimbali wakiwemo walimu, wanahabari, wanadiplomasia, wanasheria, wahandisi, wataalamu wa uchumi ukiwemo wewe Mgeni wetu Rasmi, n.k.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Seminari inapofikia miaka 41 tunawashukuru wote waliochangia kwa namna moja au nyingine mafanikio yake: tukianzia Maaskofu wamiliki wa Seminari, wafadhili wetu wa ndani na nje, kamati ya wazazi na marafiki wa Seminari, wanafunzi waliosoma hapa (St. Peter’s Seminary Alumni), wanafunzi, wafanyakazi na wote wale ambao wamewezesha Seminari hii kufikia hapa ilipo.
2.2. WAHUDUMU:
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kwa sasa Seminari ina wahudumu hamsini na moja (51) wakiwemo mapadri 7, watawa wa kike 5, walimu walei 19 na wafanyakazi Walei wasio walimu 20.
2.3. MAENDELEO YA TAALUMA:
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, historia inaonesha kuwa Seminari Ndogo ya Mt. Petro , Morogoro ni moja kati ya shule bora Tanzania kwa wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao ya Taifa. Pamoja na ukweli kuwa kuna nyakati tunashuka, lakini daima kiwango cha taaluma ni kizuri.
2.4. CHANGAMOTO:
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Utume wa Seminari Ndogo ya Mt. Petro , Morogoro tangu iasisiwe ni kutoa elimu bora ya sekondari na malezi bora kwa vijana wenye mwelekeo wa kuwa mapadri kwa gharama nafuu ambayo hata familia zenye kipato kidogo wanaweza kuimudu. Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, Morogoro ni moja ya shule zenye kiwango kidogo sana cha ada miongoni mwa shule za bweni za kulipia.
Kwa sasa kiwango cha ada kinachotolewa kinakidhi 70% ya gharama za kawaida za kuendesha shule bila kuingiza mipango ya maendeleo na ukarabati mkubwa. Hii ina maana kwamba 30% ya gharama za kuendesha shule lazima zipatikane kutoka vyanzo vingine kama miradi ya shule na misaada ya wahisani.
Mara nyingi shule imeshindwa kupata hiyo 30% ya bajeti toka vyanzo hivyo. Misaada ya wahisani haizidi 15% ya bajeti ya shule; na miradi ya shule inachangia 2% tu ya bajeti hiyo. Mbaya zaidi, karibu kila mwaka wanafunzi 20 hushindwa kabisa kulipa ada, hii ni sawa na 4% ya bajeti ya shule. Hii ina maana kuwa kila mwaka, shule inakuwa na upungufu wa 17% katika bajeti yake na hii ni kwa ajili ya gharama za kawaida tu za kuendesha shule, bila kuingiza mipango ya maendeleo na ukarabati mkubwa.
Hivyo pamoja na nia nzuri ya Seminari kutoa elimu na malezi bora kwa gharama nafuu, Seminari imejikuta katika wakati mgumu kiuchumi. Bajeti ya shule inakuwa ndogo na hivyo kuathiri mambo mengi, kama vile:
· Kukosa uwezo wa kuboresha chakula cha wanafunzi
· Kukosa uwezo wa kutoa mishahara mizuri kwa walimu na wafanyakazi wasio walimu.
· Kukosa uwezo wa kukarabati mejengo ya shule na kuyaweka katika hali bora.
· Kukosa uwezo wa kununua vitabu vya kiada na rejea vya kutosha kwa matumizi ya wanafunzi na walimu
· Kukosa uwezo wa kununua kompyuta kwa ajili ya kufundishia somo la kompyuta.
2.5. MATAZAMIO YETU:
Tukiwa na uchumi imara Seminari itakuwa katika nafasi ya kuendelea na utume wake wa kutoa elimu bora ya sekondari na malezi bora kwa vijana wenye muelekeo wa kuwa Mapadre kwa gharama nafuu inaoweza kulipwa hata na familia zenye kipato cha chini.
Hivyo, wakati Seminari inaendelea kusisitiza na kukusanya ada kutoka kwa wanafunzi, wakati Seminari inabuni na kutekeleza miradi ya kiuchumi, ni muhimu pia kuomba wahisani ndani na nje, mashirika, vikundi na mtu mmoja mmoja ambao wanaamini katika utume wa Seminari hii ili waungane nasi katika utume huu.
Tunawashukuru sana wanafunzi waliosoma hapa zamani (St. Peter’s Seminary Alumni) ambao kwa namna ya pekee hivi karibuni wameamua kusaidia maendeleo ya Seminari hii. Kwa muda mfupi tangu walipoanza rasmi kutekeleza azma hiyo hapo Januari 12, 2010 wameisaidia Seminari kwa mambo mengi kama vile:-
· Kununua meza mbili za mpira wa meza (table tennis) na seti zake (rackets) vyenye kiwango cha Olympics vikiwa na thamani ya Tshs 1,931,000.-
· Kuchangia uanzishwaji upya wa shamba la matunda; tayari miche elfu moja (1,000) ya michungwa na miembe imeshapandwa.
· Vitabu vya kiada na rejea vyenye thamani ya Tshs. 6,376,000.- vimenunuliwa na kutolewa zawadi kwa Seminari.
· Meza 13 za mninga na viti vya kisasa vya ofisini 23 vyenye thamani ya Tshs 1,800,000.- vimetolewa zawadi kwa Seminari.
· Mradi wa Biogas wenye thamani ya T.shs 12,427,750.- umeshaanza kutengenezwa kwa matumizi ya jiko la wanafunzi.
2.6. MIKAKATI YA KIUCHUMI:
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, ili kukabiliana na changamoto za kiuchumi zilizopo mbele yetu, Seminari imeazimia yafuatayo kama mpango wa kujinasua kiuchumi:
(i) Mradi wa Trekta:
Kwa kuwa chakula cha wanafunzi peke yake kinagharimu sehemu kubwa ya bajeti ya shule (23%) tumeamua ni vyema Seminari ikawa na shamba lake na hivyo kuzalisha sehemu kubwa ya chakula cha wanafunzi.
Seminari ina mpango wa kupata ekari 50 huko Kilombero kwa ajili ya kilimo cha mpunga. Matazamio yetu ni kwamba hizo ekari 50 zitatupatia kilo 30,000 za mchele, ambazo ni chakula tosha kwa mwaka na zaidi.
Matarajio yetu ni kwamba mazao yatakayopatikana na pesa itakayopatikana kutokana na kazi za trekta kwa pamoja zitachangia 16% ya bajeti ya shule.
Tayari utafiti wa aina bora ya trekta na bei yake vimeshafanywa. Trekta na jembe pamoja vinagharimu US $ 47,444.- sawa na Tshs 74,166,000.-
Seminari tayari ipo katika mchakato wa kutafuta wahisani wa kutusaidia katika hili.
(ii) Mradi wa mifugo (Nguruwe):
Aidha, Seminari imedhamiria kuboresha mradi wa mifugo, hususan kitengo cha nguruwe. Lengo letu likiwa ni kufuga kibiashara nguruwe 228. Kwa sasa mabanda yetu yana uwezo wa kuchukua nguruwe 128; kufikia lengo la nguruwe 228 tumepanga kuongeza banda la kuchukuwa nguruwe 100 zaidi.
Kwa zoezi hili tunatazamia kuboresha chakula cha wanafunzi na kupata pato ambalo kwa pamoja kwa gharama za sasa ni sawa na faida ya Tshs 41,208,240.- kwa mwaka, sawa na 11% ya bajeti ya shule.
Ujenzi wa banda jipya la nguruwe utagharimu Tshs 9,403,425.-
Wakati tukiendelea kutafuta wahisani wa kutusaidia ujenzi huo, tayari tumeshaanza kuboresha mifugo iliyopo na kuongeza idadi ya nguruwe ili kujaza mabanda yaliyopo. Hadi sasa shule ina nguruwe 73. Hivyo tuna upungufu wa nguruwe 55 kujaza mabanda yaliyopo.
2. 7. MWISHO:
Safari ni ndefu na magumu ni mengi, lakini tutafanikiwa kama tukizingatia msemo wa kiswahili “umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”.
Kwa moyo wa dhati tunawomba wote wenye kuamini na kuthamini pamoja nasi utume wa Seminari hii tuendelee kuwa kitu kimoja tuiendeleze Seminari yetu. “Penye nia pana njia”. Tukifanya kazi bega kwa bega kwa ushirikiano wa dhati tutaifanya Seminari hii kuwa bora katika kila nyanja na hivyo kutoa wahitimu bora watakaolitegemeza Kanisa na jamii kwa ujumla.
3. HITIMISHO:
Napenda kuhitimisha taarifa hii kwa kukushukuru tena Mheshimiwa Mgeni Rasmi kwa kuwa nasi katika siku hii ya leo. Wageni wengine wote, wahafarishwa wetu, wafanyakazi wote na Waseminaristi wote mnaobaki tunawashukuru sana kwa kuifanya siku hii kuwa nzuri, Mungu awabariki sana.
No comments:
Post a Comment